Friday, August 8, 2014

AZAM FC KAMA DENMARK, INAWEZA KUSHINDA KAGAME CUP…

AZAM1
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
 Yanga SC wamejitoa katika muda mbaya, lakini Azam FC wameingia katika muda maalumu na michezo yao ya tatu ya kombe la Kagame inaweza kuwa ya mafanikio licha ya kupata nafasi hiyo siku tano kuelekea ufunguzi wa michuano hiyo ya mabingwa wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Mwaka, 1992 baada ya iliyokuwa nchi ya Yugoslavia kukumbwa na balaa la vita, timu ya kandanda ya Taifa ilipoteza nafasi yake katika michuano ya ulaya, Euro, 1992 na hivyo Shirikisho la soka barani Ulaya, UEFA wakaipatia nafasi hiyo nchi ya Denmark ambayo ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Yugoslavia katika michezo ya kuwania kufuzu.
 Shirikisho la soka la nchi hiyo lilifanya kuwaita wachezaji waliokuwa rikizo baada ya kumalizika kwa ligi za Ulaya. Bila kutarajiwa, Denmark ilifanikiwa kutwaa ubingwa huo na kuwaacha mashabiki wa soka kutoamini kilichotokea. Azam hawapo katika ‘ umbo’ kama la Denmark lakini namna walivyoipata nafasi hiyo inafanya kuwepo na mfanano mkubwa, huku Azam wakiwa na faida ya ziada kwa sababu wanakwenda katika michuano huku wakiwa na maandalizi ya mwezi mmoja. Wachezaji wana usongo na hamu ya kucheza mechi za ushindani.
 Azam itakuwa uwanjani jioni ya leo katika uwanja wa Nyamahoro, Kigali, Rwanda katika mchezo wa ufunguzi wa michuano dhidi ya mabingwa wa mwaka, 1998 na moja kati ya timu wenyeji. Rayon imetwaa ubingwa wa Kagame mara moja na walifanya hivyo baada ya kuishinda, Mlandege ya Tanzania Visiwani kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali miaka 17 iliyopita. Azam imekurushwa ghafla lakini ni timu yenye uchu wa mataji. Baada ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu uliopita, timu hiyo inahitaji mafanikio zaidi katika ukanda wa CECAFA.
  KIKOSI KILICHOSHIBA, KIGALI…..
Hii ni michuano ya pili kwa Azam kushiriki na walifanikiwa kufika hatua ya fainali na kufungwa na Yanga mabao 2-0 msimu uliopita. Wachezaji wote wapo tayari kwa michuano na ushindani ni mkubwa sana, ila wote wana lengo moja. Dhidi ya wenyeji, Rayon itakuwa ni mechi ngumu sana lakini tayari kuna uzoefu wa kuzishinda timu kubwa za ukanda huu. Waliweza kuzitoa, Simba na AS Vita katika hatua za robo na nusu fainali miaka miwili iliyopita.
 Aishi Manula na Mwadini Ally wote ni makipa wazuri na watategemewa kuongoza safu ya ulinzi wakishirikiana na Shomari Kapombe ambaye atakuwa akicheza michuano yake ya kwanza kama mchezaji wa Azam, mlinzi wa kushoto, Wazir Salum na mabeki wa kati, Said Mourad na Aggrey Morris. Lolote linaweza kutokea lakini safu ya ulinzi ya Azam itakuwa sehemu ya mafanikio katika timu hiyo na mchezo wa leo unaweza kuwa sehemu ya kocha, Patrick Omog na wasaidizi wake, Kally Ongalla na Ibrahim Shikanda kujua ni namna wanaweza kujihimarisha kiumakini, kiufundi na mbinu katika michezo ya kimataifa.
  Azam wataitumia michuano hiyo ili kujiandaa na msimu ujao wa ligi kuu Tanzania Bara, ikiwa na wachezaji wapya kama, Joseph Peterson, Leonel Saint-Preux ambao ni raia wa Haiti, Mrundi, Didier Kavumbagu na wachezaji vijana kama, Abdallah Kheri, Gadiel Michael, Mudathir Yahya, Farid Mussa ni wazi michuano hiyo imekuja wakati mwakafaka kwa benchi la ufundi ukizingatia ligi kuu imesogezwa mbele kwa mwezi mmoja zaidi.
 Rayon imekuwa timu inayopewa nafasi ya kutwaa ubingwa kila michuano hiyo inapokuwa ikifanyika nchini, Rwanda lakini ubingwa wao pekee wameutwaa katika uwanja wa Amani, Zanzibar. Timu hiyo inafundishwa na kocha, Jean Francois Losciuto raia wa Ubelgiji inacheza zaidi mchezo wa kushambulia kupitia pembeni ya uwanja lakini si wazuri katika ngome. Mechi dhidi ya Azam itaonyesha kitu gani ambacho wenyeji hao wanaweza kufanya, itakuwa mechi ngumu kwa kila timu. Azam inaweza kushangaza kama Denmark mwaka 1992 walipopewa nafasi dakika za mwisho na kwenda kutwaa ubingwa wa ulaya? Tusubiri na tuone…

0 comments:

Post a Comment